Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe. Samia Suluhu Hassan ashiriki  Mkutano wa 41 wa Wakuu wa Nchi na Serikali wa Jumuiya ya Maendeleo Kusini mwa Afrika (SADC) uliofanyika tarehe 17 – 18 Agosti,2021.

Mara baada ya kuwasili katika Uwanja wa Ndege wa Kimataifa wa Kamuzu, Mhe. Rais Samia amepokelewa na Mhe. Patricia Kaliati, Waziri wa Maendeleo na Ustawi wa Jamii wa Malawi.

Katika siku ya kwanza ya mkutano huo Mhe. Rais Samia alijitambulisha rasmi kwa Wakuu wa Nchi na Serikali wa Jumuiya hiyo.

Katika hotuba yake, Mhe. Rais Samia amesema Malawi ni Taifa la kwanza  katika nchi za SADC kuongozwa na Rais Mwanamke, hivyo kujitambulisha kwake katika mkutano huo kutaongeza msukumo kwa wanawake wengi zaidi kujiamini na kuhamasika kushiriki kwenye vyombo vya maamuzi.

Mhe. Rais Samia amewasihi viongozi wa SADC kushirikiana katika kuendeleza jitihada za kuwainua na kuwawezesha wanawake katika ngazi mbalimbali za uongozi na maamuzi katika nchi zao na kuahidi kutoa ushirikiano ili kusukuma ajenda za utengamano, kushughulikia changamoto na kutekeleza mipango na mikakati mbalimbali ya maendeleo.

Katika mkutano huo, Wakuu hao wa Nchi na Serikali wamewapongeza Wananchi na Serikali ya Jamhuri ya Zambia kwa kufanya uchaguzi Mkuu na kumpongeza Rais Mteule Mhe. Hakainde Hichilema kwa kuibuka mshindi.

Viongozi hao wa SADC wamepokea taarifa kuhusu hali ya Usalama katika jimbo la Cabo Delgado Kaskazini mwa Msumbiji na kupongeza Nchi wanachama wa SADC kwa michango yao ya kifedha iliyowezesha kupelekwa kwa Jeshi la Dharura la SADC nchini Msumbiji.

Mkutano huo wa 41 pia umeridhia mabadiliko ya Jukwaa la Bunge la SADC kuwa Bunge la SADC la ushauri na majadiliano.

Nje ya Mkutano huo, Mhe. Rais Samia amekutana na kufanya mazungumzo na Rais mstaafu wa Malawi Mhe.  Joyce Banda.

Mhe. Rais Mstaafu Joyce Banda amempa pole Mhe. Rais Samia kufuatia msiba wa Hayati Rais Magufuli na kumpongeza kwa kushika nafasi ya Urais, ambapo amemuahidi kumpa ushirikiano akiwa Rais mstaafu mwanamke.

Kwa upande wake Mhe. Rais Samia amemshukuru Rais Mstaafu Banda na kuahidi kuendeleza ushirikiano wa kidugu na wa kihistoria kati ya Tanzania na Malawi.

Mhe. Rais Samia amerejea nchini na kupokewa na Makamu wa Rais Mhe. Dkt. Philip Mpango pamoja na viongozi mbalimbali  katika Uwanja wa Ndege wa Kimataifa wa Abeid Amani Karume Zanzibar.