Tarehe 30 Aprili 2026.Mawaziri wa nchi Wanachama wa Umoja wa Afrika wanaoshughulikia masuala ya Nishati na Uchukuzi wamempendekeza rasmi Mheshimiwa Dkt. Samia Suluhu Hassan, Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania kuwa Kinara wa Afrika (Champion) wa ajenda ya nishati safi ya kupikia.

Hatua hiyo imetikiwa wakati wa Mkutano wa 5 wa Mawaziri wa nchi Wanachama wa Umoja wa Afrika unaoshughulikia Nishati na Uchukuzi, uliofanyika jijini Johannesburg, Afrika Kusini. Katika Mkutano huo, Ujumbe wa Tanzania katika ngazi ya Mawaziri uliongozwa na Mheshimiwa Deogratius Ndejembi (Mb), Waziri wa Nishati. Aidha, Mhe. James G. Bwana, Balozi wa Tanzania nchini Afrika ya Kusini alikuwa sehemu ya Ujumbe ulioambatana na Mheshimiwa Waziri Ndejembi (Mb). Akizungumza katika mjadala kuhusu Programu ya Nishati Safi ya Kupikia Afrika, Mheshimiwa Ndejembi alieleza kuwa mafanikio ya Tanzania katika sekta hiyo yametokana na uongozi madhubuti wa Mheshimiwa Dkt. Samia Suluhu Hassan katika kusukuma ajenda ya nishati kupikia ndani na nje ya nchi.

Pendekezo hilo ni ishara ya kutambua mchango wake mkubwa katika kuhamasisha na kuendeleza matumizi ya nishati safi ya kupikia ndani na nje ya nchi, sambamba na juhudi za kupunguza athari za kiafya na kimazingira na kuboresha maisha ya Wananchi wa Afrika, hususan Wanawake na Watoto. Katika ngazi ya wa Wataalam, ushiriki wa Tanzania uliongozwa na
Kamishna wa Umeme na Nishati Jadidifu, Mhandisi Innocent Luoga, aliyekuwa akiongoza ujumbe wa sekta katika majadiliano ya kimkakati yanayolenga kuimarisha maendeleo ya miundombinu ya nishati na uchukuzi Barani Afrika. Wataalam wengine walioshiriki ni Bi. Stella Katondo, Mkurugenzi wa Usalama wa Usafiri na Mazingira wa Wizara ya Uchukuzi, Bw. Mohamed Salum, Mkurugenzi Mkuu wa TASAC na Bi. Happiness Godfrey, Mwambata Bishara na Uwekezaji Ubalozini.