MAKALA MAALUMU YA ZIARA YA KISERIKALI YA MHESHIMIWA  DKT. SAMIA SULUHU HASSAN, RAIS WA JAMHURI YA MUUNGANO WA TANZANIA NCHINI AFRIKA KUSINI TAREHE 15- 16 MACHI 2023

Mheshimiwa Dkt. Samia Suluhu Hassan, Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania aliafanya ziara ya kwanza ya Kiserikali nchini Afrika Kusini kuanzia tarehe 15 – 16 Machi, 2023 kufuatia mwaliko wa Mheshimiwa Cyril Ramaphosa, Rais wa Jamhuri ya Afrika Kusini.

Ziara hiyo ililenga kuimarisha uhusiano na ushirikiano wa kidugu, kihistoria na wa kimkakati uliopo pamoja na masuala ya kiuchumi baina ya Tanzania na Afrika Kusini. Kwenye ziara hiyo Mhe.Rais Samia aliongoza ujumbe wa Viongozi mbalimbali Serikalini wakiwemo Waheshimiwa Mawaziri, Makatibu Wakuu, Watendaji Wakuu wa Serikali pamoja na wawakilishi kutoka sekta binafsi ikiwemo wafanyabiashara.

Tanzania na Afrika Kusini zina uhusiano mzuri baina yao na wa kihistoria ambao umekuwapo kati ya nchi hizi mbili tangu enzi za uhuru na mapambano ya ukombozi. Uhusiano huu wa karibu uliopo, uliimarishwa na Waasisi wa mataifa haya mawili: Hayati Mwalimu Julius K. Nyerere na Hayati Nelson R. Mandela na Oliver R. Tambo. Uhusiano wa karibu kati ya nchi hizo mbili pia umedumishwa na viongozi waliofuata kupitia ziara na kwa kuunda ushirikiano wa kina wa kiuchumi, kisiasa na kijamii.

 

RAIS SAMIA ATUNUKIWA NISHANI YA JUU YA AFRIKA KUSINI NA MWENYEJI WAKE RAIS CYRIL RAMAPHOSA

Mhe. Dkt. Samia Suluhu Hassan akitunukiwa Tuzo ya Juu Kabisa ya Heshima inayotolewa na Mhe.Cyril Ramaphosa. Mhe. Dkt. Samia Suluhu Hassan alitunukiwa tuzo hiyo ya Juu Kabisa ya Afrika Kuisni (The Order of South Africa)ikiwa ni pongezi kwa kuandika historia ya kuwa mwanamke wa kwanza kuwa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, pia ameendelea kudumisha udugu wa kihistoria wa mataifa hayo mawili, Afrika Kusini inatambua mchango wa Kijeshi, Kijamii na Vifaa, kwa Wapigania Uhuru wa Afrika Kusini uliotolewa na Tanzania wakati wa siku za kiza za ukandamizaji huko Afrika Kusini, ambapo kuanzia miaka ya mwanzo ya 1960 hadi Afrika Kusini ilipopata Uhuru, Tanzania ilikuwa nyumbani kwa wapigania Uhuru wa Afrika Kusini.

 

MAZUNGUMZO NA WAANDISHI WA HABARI

Waheshimiwa Marais waliongea na wahandishi wa Habari na kuwaeleza yaliyojiri kwenye Official Talks ikiwa ni pamoja na mashirikiano katika sekta ya biashara na uwekezaji, mashirikiano katika sekta ya utalii, matumizi ya lugha ya Kiswahili katika mfumo rasmi wa elimu nchini Afrika Kusini na kufanyika kwa Mikutano ya Mkutano wa Pili wa Tume ya Mataifa Mawili (Bi-National Commission-BNC) kati ya Tanzaniana Afrika Kusini na Kongamano la Biashara.

 

UTIAJI SAINI WA HATI ZA MAKUBALIANO

Waheshimiwa Marais wakishuhudia utiaji Saini wa Hati ya Makubaliano kati ya Wizara ya Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania na Idara ya Uhusiano na Ushirikiano wa Kimataifa ya Jamhuri ya Afrika ya Kusini (Memorandum of Understanding on Holding Political and Diplomatic Consultations na Hati ya Chuo cha Diplomasia cha Tanzania na Chuo cha Diplomasia cha Afrika Kusini

 

KONGAMANO LA BIASHARA BAINA YA TANZANIA NA AFRIKA KUSINI

Mheshimiwa Rais Samia na Mwenyeji wake Mheshimiwa Rais Ramaphosa walihudhuria na kuhutubia katika Kongamano la Biashara kati ya Tanzania na Afrika Kusini. Kongamano hilo la Biashara lilikuwa na jumla ya washiriki 350 kutoka pande zote mbili.Sambamba na komgamano hilo kulikuwa na maonyesho ya bidhaa mbalimbali zipatikanazo Tanzania na Afrika Kusini Mada kuu ya Kongamano Kaulimbiu ya Kongamano hilo ambalo lilishirikisha sekta za kilimo, madini, Mafuta na gesi, miundombinu, viwanda, biashara, uwekezaji nishati ni “Forging a new deal between South Africa and Tanzania Towards High Levels of Trade and Investments”.
Tanzania na Afrika Kusini zimekuwa katika ushirikiano wa kibiashara na kiuchumi kwa miongo mingi. Ushirikiano huo unaimarishwa zaidi na uwepo wa Jumuiya ya Maendeleo Kusini mwa Afrika (SADC). Nchi zote mbili pia ni Wanachama wa Eneo Huria la Biashara la Utatu, AfCFTA na Shirika la Biashara Ulimwenguni.

Afrika Kusini ni miongoni mwa nchi 10 zilizowekeza kwa wingi nchini Tanzania na inachukua takriban 10% ya uwekezaji wote nchini Tanzania. Kwa mujibu wa Kituo cha Uwekezaji Tanzania (TIC), hadi kufikia Desemba 2022, Tanzania tunayo jumla ya makampuni 226 kutoka Afrika Kusini yenye thamani ya Dola za Marekani 1,063.91 milioni. Kampuni hizo zimeajiri zaidi ya watanzania 21,075.  Kutokana na mabadiliko ya kiuchumi, miundombinu na kidiplomasia inayofanywa na Serikali ya Awamu ya 6, inatarajiwa idadi hii itaongezeka kwa kuwa wawekezaji wengi wa Afrika Kusini wameonyesha nia na wanatafuta fursa za uwekezaji nchini Tanzania. Orodha kamili ya miradi ya Uwekezaji ya Afrika Kusini nchini Tanzania.

Biashara Kati ya Tanzania na Afrika Kusini

Kwa miaka kumi na tano mfululizo kiwango cha biashara kati ya Afrika Kusini na Tanzania kimekuwa kikiongezeka kutoka dola za Kimarekani milioni 976,331 mwaka 2007 hadi dola milioni 2,928,242.9 mwaka 2021; na katika kipindi hicho urari wa biashara ya Tanzania ulikuwa chanya (isipokuwa mwaka 2013). Bidhaa za Tanzania zinazouzwa Afrika Kusini ni pamoja na Mashine, madini ya chuma, chai nyeusi, maua, tumbaku, dhahabu, kahawa, korosho, vegetable fats na pamba.

Bidhaa kutoka Afrika Kusini zinazouzwa Tanzania ni pamoja na: Vifaa vya mitambo mbalimbali, Karatasi, bidhaa za mpira, trekta, Magari ya chuma Malori ya Kusafirisha mizigo, Trela na nusu-trela, mvinyo, maepo, makopo ya mvinyo, makaa ya mawe, vipeperushi, vitabu vilivyochapishwa, magari, mashine mbalimbali, pampu za vimiminika, Takwimu za biashara baina ya Tanzania na Afrika Kusini.

 

MATUKIO MBALIMBALI WAKATI WA KONGAMANO LA BIASHARA

Wakati wa Kongamano hilo mada mbalimbali ziliwasilishwa kutoka kwa wataalam wa pande zote mbili ambapo washiriki watapata fursa ya kujadiliana na kubadilishana uzoefu ikiwa ni pamoja na mazingira ya biashara na uwekezaji; fursa na changamoto zinazowakabili na kutoa suluhisho la namna ya kukabiliana nazo; fursa ya kuimarisha ushirikiano katika kilimo na usindikaji wa mazao ya kilimo; sekta ya gesi na fursa za kuimarisha uhusiano wa mnyororo wa thamani; uchimbaji madini na faida zake;miradi muhimu ya ujenzi na miundombinu; na fursa zilizopo nchini Tanzania (reli, Dodoma Master Plan, nishati). Pia, washiriki walipata fursa ya kufanya mikutano ya kibiashara (business to business meetings) ambayo iliwasaidia kutengeneza mitandao na kupata masoko ya bidhaa zao.

 

MHESHIMIWA RAIS DKT. SAMIA SULUHU HASSAN ATEMBELEA FREEDOM PARK MAKUMBUSHO YA UHURU WA AFRIKA KUSINI

Mheshimiwa Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan atembelea Freedom Park makumbusho ya Uhuru wa Afrika Kusini ambayo yalianzishwa kwenye misingi ya utu, haki na uhuru wa binadamu na inaonyesha mafanikio ya kujitolea ya Afrika Kusini kama taifa. Eneo hilo lililosheheni historia ya Afrika Kusini linatambua mchango wa nchi mbalimbali ikiwemo Tanzania katika kufanikisha ukombozi wa Afrika Kusini.

Akiwa katika makumbusho hayo Mheshimiwa Dkt. Rais Samia Suluhu Hassan aliweka shada la maua kwenye Ukuta wa Majina ambao ni kumbukumbu yenye orodha ya majina ya waliopoteza maisha wakati wa migogoro mikubwa katika historia ya Afrika Kusini, ikiwa ni pamoja na mauaji ya halaiki, Vita Kuu ya I na II ya dunia na vile vile wakati wa utawala wa ubaguzi wa rangi. Ukuta huo una takriban majina 75,000. Aidha, katika hatua hiyo ya uwekaji shada la maua Mhe.Rais Samia alipokelewa na Silent guard.  

 

MATUKIO MENGINEYO:

Mkuu wa Kitivo cha Sayansi ya Usimamizi, Dk Edgar Nesamvuni na Dk Florian Mtey, Makamu Mkuu wa Chuo cha Taifa cha Utalii(NCT) - Tanzania wasaini Hati ya Makubaliano ya Ushirikiano (MoU) baina ya Chuo cha Taifa cha Utalii na Chuo cha Teknolojia cha Tshwane- Afrika Kusini.TUT na NCT zinalenga kufanya kazi pamoja katika maeneo yafuatayo;
i. Utoaji wa pamoja wa programu katika nyanja za Usimamizi wa Utalii;
ii. Usimamizi wa Matukio, Usimamizi wa Ukarimu na Maendeleo ya Ujasiriamali;
iii. Kubadilishana kwa watumishi kama wahadhiri wageni katika fani zao za Usimamizi wa Utalii, Usimamizi wa Matukio, Usimamizi wa Ukarimu na Maendeleo ya Ujasiriamali kama ilivyokubaliwa pindi inapotokea;
iv. Kubadilishana kwa wanafunzi kwa vipindi kama ilivyokubaliwa katika makubaliano tofauti na utambuzi wa moduli zilizokamilishwa za masomo kwa madhumuni ya kufuzu kwa kuzingatia viwango vya Mfumo wa Kitaifa wa Sifa za nchi husika;na
v. Utoaji wa msaada kwa wanafunzi kufanya kazi za mradi katika taasisi zote mbili.

 

KIKAO CHA KUJADILI MIPANGO WA UTEKELEZAJI WA MAKUBALIANO YA USHIRIKIANO WA MAENDELEO YA ELIMU YA MSINGI BAINA YA WIZARA YA ELIMU, SAYANSI NA TEKNOLOJIA; WIZARA YA ELIMU NA MAFUNZO YA AMALI ZANZIBAR NA WIZARA YA ELIMU YA MSINGI YA AFRIKA KUSINI.
  
Bw. Ali Khamis Juma  Katibu Mkuu, Wizara ya Elimu na Mafunzo ya Amali Zanzibar  na Prof. James Epiphany Mdoe. Naibu Katibu Mkuu Wizara ya Elimu, Sayansi na Teknolojia  walikutana na Bi. Simone Geyer, Naibu KAtibu Mkuu,Wizara ya Elimu ya Msingi ya Afrika Kusini na kujadili maendeleo ya mipango ya utekelezaji wa Makubaliano ya Ushirikiano wa MAendeleo ya Elimu ya Msingi baina ya Wizara ya Elimu,Sayansi na Teknolojia;Wizara ya Elimu na Mafunzo ya Amali Zanzibar na Wizara ya Elimu ya Msingi ya Afrika Kusini.
Itakumbukwa kuwa tarehe 7 Julai 2022 Tanzania na Afrika Kusini zilisaini Hati ya Makubaliano ya Ushirikiano (MoU) kwenye elimu ya msingi ikiwa ni pamoja na ufundishaji wa kiswahili katika shule za msingi za Afrika Kusini. Utiaji Saini huo ulishuhudiwa na Mhe. Dkt.Philip Mpango, Makamu wa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania pamoja na  Mhe. Prof Adolf Mkenda (Mb), Waziri wa Elimu, Sayansi na Teknolojia na Mhe. Matsie Angelina Motshekga, Waziri wa Elimu ya Msingi wa Afrika Kusini.

TATHMINI

MAFANIKIO YA ZIARA


BAADHI YA FURSA ZINAZOPATIKANA KATIKA ENEO LA UWAKILISHI
      
Soko la Parachichi: Novemba 2021 Mamlaka ya Hifadhi ya Chakula Tanzania (NPPC) na Mamlaka ya Hifadhi ya Chakula ya Afrika Kusini (NPPZA) walitia saini makubaliano ya kuruhusu Parachichi za Tanzania kuuzwa katika soko la Afrika Kusini. Afrika Kusini ndiyo mzalishaji mkubwa wa parachichi, ingawa msimu wa kuanzia Septemba hadi Machi kila mwaka hawana mavuno, hivyo wanategemea kuagiza matunda hayo kutoka nchi nyingine. Mwezi Januari 2023 Mfanyabiashara wa mmoja wa Kitanzania Bw. Michael Ngogo amesafirisha maparachichi tani 2 kutoka Tanzania na kuyaleta nchini Afrika Kusini.

Soko la Mchele: Afrika inaagiza chakula chenye thamani ya zaidi ya Dola za Marekani (USD) bilioni 35 kwa mwaka, ambapo dola bilioni 7 hununua mchele kutoka Asia na sehemu nyingine za dunia. Nchi za SADC huagiza mchele wenye thamani ya zaidi ya dola bilioni 1 kila mwaka kutoka nje ya Afrika. Mchele unaopatikana Afrika Kusini na nchi jirani unatoka nchi za Asia. Tanzania inazalisha tani milioni 2.2 za mpunga kila mwaka, ambapo tani 900,000 ni kwa ajili ya mahitaji ya ndani, na ziada inaweza kuuzwa nje ya nchi. Uzalishaji huo unafanyika katika hekta 600,000 pekee kati ya hekta milioni 21 zinazoweza kulimwa kwa mpunga. Hivyo, hii ni fursa nzuri kwa Tanzania kupanua uzalishaji wake na kufikia soko la nchi za SADC.

Mbegu bora za ng’ombe na mbuzi: Afrika Kusini ina mbegu bora za ng'ombe na mbuzi zinazoweza kufugwa nchini Tanzania. Ni vyema Wizara ya Mifugo na Taasisi za Utafiti zikashirikiana kuwasaidia wafugaji kupata mbegu hizo.

Soko la maharagwe ya sukari: Bidhaa hii ni adimu katika eneo la uwakilishi na hutafutwa sana nchini Tanzania. Wafanyabiashara wa Afrika Kusini bado hawajapata kiasi cha kutosha na cha kuaminika cha bidhaa. Kwa sasa Tanzania inazalisha tani 300,000 tu za maharage ya sukari kwa mwaka. Kwa kuwa Tanzania ina ardhi nzuri yenye rutuba, ni fursa kwa nchi yetu kuongeza uzalishaji ili kuhudumia soko la SADC na Asia pia.

Soko la korosho na tangawizi: Korosho na tangawizi za Tanzania zinahitajika katika eneo la uwakilishi. Tangawizi ya Tanzania ina ubora wa hali ya juu kuliko ile inayopatikana sehemu nyingine, hivyo ni fursa kwa nchi yetu kufanya mikataba ya kibiashara ya mazao ya kilimo kuyauza Afrika Kusini na nchi jirani.

Fursa za mafunzo: Afrika Kusini ina vyuo vikuu vingi bora barani Afrika, lakini taratibu mahususi zinaendelea ili kuwa na makubaliano ya ushirikiano katika elimu ya juu ili kufaidika na uwepo wa vyuo vikuu hivi. Aidha, Afrika Kusini pia ina vyuo vingi vya kufundisha urubani, na Watanzania wengi hushiriki katika mafunzo hayo.
Sambamba na hilo, kuna fursa ya kufundisha Kiswahili kwa wanafunzi wa awali (beginers) hivyo, tunahamasisha walimu wa Kiswahili kutumia fursa hiyo ambayo madarasa yake yanaweza kufanyika hata kwa njia ya mtandao.

Mazao ya Kilimo: Idadi ya watu wa Afrika Kusini inaongezeka kila siku, na mahitaji ya chakula ni  makubwa. Pia, hakuna usambazaji wa kutosha kulisha Waafrika Kusini wote, jambo ambalo linalazimisha Serikali na makampuni mengine ya kibinafsi kuagiza kutoka nchi jirani. Shinikizo la upatikanaji wa chakula cha kutosha linahitaji uwekezaji wa kilimo kwa usalama wa chakula wa siku zijazo. Hii ni fursa kwa wawekezaji kufungua kampuni binafsi ya kilimo kwa ajili ya mazao, matunda, na uzalishaji wa mbogamboga. Aidha,  wafanyabiashara wanaweza kuleta bidhaa za chakula kama chai, kahawa,korosho, mchele,maharage, ulezi,maparachichi n.k.

Ufugaji wa Samaki: Kuna ongezeko la mahitaji ya nyama ya samaki na chakula cha majini nchini Afrika Kusini kwa sababu ya faida zake za kiafya. Mahitaji ya wenyeji ya nyama ya samaki na mafuta ni makubwa, na usambazaji ni mdogo, lakini samaki wengi nchini Afrika Kusini wanauzwa nje, na kuwaacha wenyeji bila samaki kwenye sahani zao. Bado kuna fursa kubwa ya uwekezaji wa ufugaji wa samaki nchini kwa samaki na milo ya samaki kama mahindi na ngano

 

 

 

Matukio ya Picha

  • Mheshimiwa Dkt.Samia Suluhu Hassan akipokea maua kutoka kwa mtoto Malaika Adam Issara mara tu alipowasili hotelini.
  • Mheshimiwa Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan akiimba pamoja na baadhi ya jumuiya ya Watanzania waishio nchini Afrika Kusini (Diaspora).
  • Mheshimiwa Dkt. Rais Samia Suluhu Hassan akipokelewa rasmi katika Ikulu ya Afrika Kusini na mwenyeji wake Mheshimiwa Cyril Ramaphosa, Rais wa Jamhuri ya Afrika Kusini.
  • Mheshimiwa Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan alikagua gwaride la heshima na kupigiwa mizinga ishirini na moja (21) mara baada ya kuwasili katika viwanja vya Mapokezi ya Viongozi vilivyopo kwenye Majengo ya Union Buildings,Ikulu Afrika Kusini.
  • Mheshimiwa Rais Ramaphosa akisalimiana na Waheshimiwa Mawaziri walioambatana na Mheshimiwa Rais Samia.
  • Mheshimiwa Rais Samia akisalimiana na Waheshimiwa Mawaziri walioambatana na Mheshimiwa Rais Ramaphosa.
  • Mazungumzo Ya Faragha (tête-à-tête)
  • Baada ya sherehe ya mapokezi, Mheshimiwa Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan alifanya mazungumzo ya faragha (tête-à-tête) na Mwenyeji wake Rais Cyril Ramaphosa.
  • Mheshimiwa Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan na mwenyeji wake na kushiriki Mazungumzo ya Pande Mbili (Official Talks) yaliyohusisha Mawaziri na baadhi ya Watendaji Wakuu wa Serikali.
  • Rais Samia Atunukiwa Nishani Ya Juu Ya Afrika Kusini Na Mwenyeji Wake Rais Cyril Ramaphosa
  • Waheshimiwa Marais waliongea na wahandishi wa Habari na kuwaeleza yaliyojiri kwenye Official Talks ikiwa ni pamoja na mashirikiano katika sekta ya biashara na uwekezaji, mashirikiano katika sekta ya utalii, matumizi ya lugha ya Kiswahili katika mfumo rasmi wa elimu nchini Afrika Kusini na kufanyika kwa Mikutano ya Mkutano wa Pili wa Tume ya Mataifa Mawili (Bi-National Commission-BNC) kati ya Tanzaniana Afrika Kusini na Kongamano la Biashara.
  • Waheshimiwa Marais wakishuhudia utiaji Saini wa Hati ya Makubaliano kati ya Wizara ya Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania na Idara ya Uhusiano na Ushirikiano wa Kimataifa ya Jamhuri ya Afrika ya Kusini (Memorandum of Understanding on Holding Political and Diplomatic Consultations na Hati ya Chuo cha Diplomasia cha Tanzania na Chuo cha Diplomasia cha Afrika Kusini.
  • Waheshimiwa Marais wakihutubia Kongamano la biashara.
  • Waheshimiwa Marais wakihutubia Kongamano la biashara.
  • Waheshimiwa Marais walishuhudia utiaji saini wa Hati ya Makubaliano ya Ushirikiano kati ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania na Jamhuri ya Afrika Kusini katika nyanja ya Viwanda na Biashara
  • Wafanyabiashara mbalimbali wakionyesha bidhaa zao wakati wa Kongamano la Biashara lililosheheni wafanyabiashara kutoka Tanzania na Afrika Kusini wenye nia ya kupanua wigo wa biashara zao.
  • Mheshimiwa Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan Atembelea Freedom Park Makumbusho Ya Uhuru Wa Afrika Kusini
  • Mheshimiwa Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan akutana kwa mazungumzo na Mheshimiwa Paul Mashatile, Makamu wa Rais wa Jamhuri ya Afrika Kusini. Mheshimiwa Mashatile alikutana na Mheshimiwa Rais kwa lengo la kumsalimu na kujitambulisha kwa kuzingatia kuwa ameteuliwa siku chahe tu kabla ya ziara hiyo kufanyika.