Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania na Amiri Jeshi Mkuu Mhe. Samia Suluhu Hassan, afungua Mkutano wa Tano wa Mkuu wa Majeshi ya Ulinzi na Makamanda wa Jeshi la Wananchi wa Tanzania leo tarehe 15 Novemba, 2021
Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania na Amiri Jeshi Mkuu Mhe. Samia Suluhu Hassan, leo tarehe 15 Novemba, 2021 amefungua Mkutano wa Tano wa Mkuu wa Majeshi ya Ulinzi na Makamanda wa Jeshi la Wananchi wa Tanzania (JWTZ) na kuwapongeza Maafisa na Askari wote wa Jeshi hilo kwa kazi nzuri wanayofanya ya kulinda Taifa na mipaka yake.
Mhe. Rais Samia pia amevipongeza vyombo vyote vya ulinzi na usalama kwa kazi nzuri wanayofanya na kuwezesha taifa kuvuka salama baada ya msiba wa aliyekuwa Rais wa Awamu ya Tano na Amiri Jeshi Mkuu, Hayati Dkt. John Pombe Magufuli.
Rais na Amiri Jeshi Mkuu, Mhe. Samia amesema ndani ya miaka 60 Jeshi letu limefanya kazi nzuri ya kulinda na kusimamia usalama wa mipaka yetu na uhuru wa nchi ambayo ni nyenzo muhimu sana kwa maendeleo yetu ya kiuchumi, kisiasa na kijamii.
Aidha, Rais na Amiri Jeshi Mkuu, Mhe. Samia amesema anafahamu kuwa JWTZ kwa kushirikiana na vyombo vingine vya ulinzi na usalama nchini vina sifa zote za ubora, umakini na uimara unaoiletea sifa Tanzania ndani na nje ya nchi.
Rais na Amiri Jeshi Mkuu, Mhe. Samia amepongeza utaratibu wa Mkutano huo unaowakutanisha mara moja kwa mwaka kujadili changamoto mbalimbali zinazowakabili na kuzitafutia ufumbuzi, hali inayowapa fursa ya kujitathmini namna gani ya kukabiliana na changamoto hizo.
Amesema Jeshi la Tanzania limekuwa la kutolea mfano kwa kanda ya Afrika Mashariki, Kusini mwa Afrika na Dunia kwa ujumla ambapo mara zote limetekeleza majukumu yote ya kitaifa na kimataifa waliyopewa kwa ufanisi, uzalendo na weledi wa hali ya juu ikiwa ni pamoja na kushiriki katika misheni za kulinda amani katika Bara la Afrika na maeneo mengine duniani.
Aidha, Rais na Amiri Jeshi Mkuu Mhe. Samia amesema Serikali imepeleka vikosi maalum katika mpaka wa Tanzania na Msumbiji katika eneo la mkoa wa Mtwara kwa ajili ya kuimarisha ulinzi na usalama, kuleta utulivu na kurejesha shughuli za kiuchumi na kijamii katika eneo hilo.
Rais na Amiri Jeshi Mkuu Mhe. Samia amelihakikishia Jeshi la Wananchi wa Tanzania (JWTZ) kuwa Serikali itatoa kila aina ya usaidizi ili kuweza kutekeleza majukumu yao kikamilifu ikiwemo jukumu la kulinda uhuru na mipaka ya Taifa dhidi ya matishio ya ndani na nje ya nchi kupitia vikosi vya nchi kavu, angani na majini.
Rais na Amiri Jeshi Mkuu Mhe. Samia pia amezitaka Taasisi mbalimbali vikiwemo vyombo vya habari na Asasi za Kiraia kushirikiana na Vyombo vya Ulinzi na Usalama kuelimisha wananchi kuhusu umuhimu wa amani na madhara ya kujihusisha na vitendo vya kigaidi.