Makamu wa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe. Samia Hassan amewasili  Mjini Windhoek Namibia leo Agosti 15, 2018 kumuwakilisha Rais wa Jamhuri ya Muungano
wa Tanzania Mhe. Dkt. John Magufuli katika Mkutano wa 38 wa Wakuu wa Nchi na Serikali wa Jumuiya ya
Maendeleo ya Kusini mwa Afrika (SADC), utakaofanyika tarehe 17 – 18 Agosti
2018.

Katika Uwanja wa Ndege wa Kimataifa wa Hosea Kutako mjini Windhoek
Namibia, Makamu wa Rais amepokelewa na  Waziri wa Elimu ya Juu , Mafunzo na Ubunifu wa
Namibia Mhe. Dkt. Itah Kandjii – Murangi , Naibu Waziri wa Mambo ya Nje na
Ushirikiano wa Kimataifa Mhe. Christin Hoebes na viongozi mbalimbali wa
Serikali ya Namibia.

Hii ni sehemu ya mikutano ya awali ya
maandalizi ya mkutano wa 18 wa Wakuu wa Nchi na Serikali wa SADC utakaofanyika
tarehe 17 na 18 Agosti 2018 mjini Windhoek, Namibia. 

Mikutano mingine ya awali ni pamoja na mkutano
wa Makatibu Wakuu wa SADC uliofanyika tarehe 9 na 11 Agosti 2018 na Mkutano wa
Wakuu wa Nchi na Serikali wa Asasi ya Ushirikiano wa Siasa , Ulinzi na Usalama
ya SADC (SADC Organ on Politics, Defence and Security) utakaofanyika tarehe 16
Agosti 2018 ambao utapitia na kujadili hali ya Siasa, Ulinzi na Usalama katika
Kanda kwa kipindi cha Agosti 2017 hadi Agosti 2018. 

Mkutano huu
utahusisha nchi tatu za SADC Organ TROIKA na wajumbe wake ambao ni Angola
Mwenyekiti wa sasa wa Asasi ya SADC ya Ushirikiano wa Siasa, Ulinzi na Usalama, Zambia ambao ni Makamu Mwenyekiti wa Organ na
Jamhuri ya Muungano wa Tanzania ambayo ni Mwenyekiti wa Organ aliyemaliza muda
wa uenyekiti wa Asasi hiyo.