Balozi wa Tanzania nchini Afrika Kusini Mhe. Sylvester Mwakinyuke Ambokile Jumamosi Juni 23, 2018 amekutana na kufanya mazungumzo na Watanzania wanaoishi nchini humo, na kuwaongoza katika kuunda umoja wao kwa mara ya kwanza, kwenye mkutano uliofanyika ubalozini jijini Pretoria.

"Sisi leo tulikuwa tunakutana na watanzania wa Afrika kusini. Ndugu zetu hawa walikuwa hawana umoja wao wa kuwaunganisha. Na ndiyo tunakutana kuujadili umoja huo ambao nimesaidia  kuaandikishwa rasmi serikalini. Umoja huo unaitwa Tanzanian  community in South Africa  (TACOSA)", Balozi Ambokile aliiambia Globu ya Jamii kwa njia ya mtandao usiku wa kuamkia leo.

Amesema ubalozi uliamua kuchukua hatua hiyo kwa kuzingatia kwamba Watanzania wengi wanaishi nchini Afrika Kusini, wengi wao wakiwa wanafunzi, wafanyabiashara na wafanya kazi lakini walikuwa hawana umoja wa kuwaunganisha  kwenye masuala mbalimbali yanayopaswa kufanywa na wana-Diaspora. 

Balozi Ambokile amesema kwamba kwa umoja huo, sasa Watanzania waishio Afrika Kusini watakuwa na fursa ya kuwa pamoja na kusaidiana katika shida na raha, tofauti na ilivyokuwa awali ambapo kila mmoja wao alikuwa akifanya mambo yake kivyake.

"Hii itaturahihishia pia kuwakusanya  pamoja katika masuala ya misiba, harusi, sherehe za Kitaifa na mengineyo kama wafanyavyo Watanzania walio katika nchi zingine" alisema Mhe. Balozi.
 

  • Sehemu ya watanzania waishio nchini nchini Afrika Kusini wakiwa kwenye mkutano uliofanyika Jumamosi Juni 23, 2018 ubalozini jijini Pretoria.
  • Watanzania waishio nchini nchini Afrika Kusini wakiwa kwenye mkutano wao na balozi uliofanyika Jumamosi Juni 23, 2018 ubalozini jijini Pretoria.